#
  • UNIVERSITY OF DAR ES SALAAM ACADEMIC STAFF ASSEMBLY (UDASA)

Article from UDASA member

Salamu za Rambirambi za Jumuiya ya Wafanyakazi Wanataaluma wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDASA)
Dr Mathew Mndeme |
Published on Sep 28, 2021

Ibada ya Mazishi ya Prof Matthew Laban Luhanga, Jumatatu Tarehe 20/ 09/ 2021
Ukumbi wa Nkurumah, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Kampasi ya Mwalimu Nyerere Mlimani
 
Naomba nimwongelee Marehemu Prof Luhanga tofauti kidogo na waombolezaji wengine na nitafanya hivyo kwa ufupi kwa kuwa wengi wameshaelezea mambo mengi mazuri kumhusu. Nitafanya hivyo kwa kuanza na moja ya hadhithi ambazo Prof Luhanga aliziitumia wakati akifundisha kuhamasisha wanafunzi wake kupenda uhandisi akiamini fani ya kipekee katika kufanikisha mambo mengi.

“Kuna wafu walipelekwa motoni/ jehanamu. Lakini cha ajabu wakawa hawaungui wakati moto ni mkali. Basi Mwenyezi Mungu akamwuliza malaika wake, vipi hawa watu mbona hawaungui? Malaika akajibu, hao ni wahandisi. Wametumia utaalamu wao kudhibiti moto wa jehanamu usiwaunguze”.

Profesa Luhanga kama MWANAUDASA
UDASA tumepoteza mwanataaluma wa mfano aliyeipenda sana kazi yake kama mhadhiri na mtafiti; tumepoteza Professa mbobezi wa fani ya mawasiliano pepe; tumepoteza mhandisi nguli, na kiongozi mwanataaluma mahiri.

Prof Luhanga aliongoza chuo chetu kama Makamu Mkuu wa Chuo kuanzia mwaka1991 hadi 2006 akiwa na miaka 42. Ndani ya kipindi hiki mambo mengi yalitokea ndani na nje ya chuo ambayo kwa namna moja au nyingine yaliamua hali na uendeshaji wa chuo uweje.

  • Kwanza, baadhi ya nchi duniani zilikua bado chini ya Ukoloni.

  • Pili, zama za vita baridi zilikua zinafikia ukingoni kupelekea kuanguka kwa Muungano wa nchi za kisoshalisti (Union of Soviet Socialist Republics - USSR).

  • Tatu, vuguvugu la kuanzishwa mfumo wa vyama vingi vya siasa Tanzania na kwingineko Afrika lilikua limeshika kasi.

  • Nne, nchi yetu iliingia kwenye chaguzi za vyama vingi vya siasa mwaka 1995, 2000 na 2005.

  • Tano, serikali ya Hayati Rais Mkapa ilibinafsisha ya mashirika ya umma na sekta binafsi kukua kwa kazi.

  • Sita, nchi ilipatwa na mtikisiko mkubwa wa kiungozi na kihistoria kufuatia kifo cha Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere mwaka 1998.

  • Nane, CKD kilikua na wanafunzi takribani elfu tatu na miundombinu isiyokidhi mahitaji, huku mahitaji ya utoaji wa elimu ya juu nchini ukiwa unaongezeka kwa kasi.

  • Saba, idadi ya wanataaluma hasa wenye elimu ya kiwango cha shahada ya uzamivu iliku ni ndogo sana huku mahitaji ya utoaji wa elimu ya juu yakiongezeka.


Mambo haya na mengine mengi, yaliwahusisha wanaUDASA kwa namna nyingi hasa kutokana na CKD kuwa na nafasi ya kipekee katika maendeleo ya nchi na harakati mbalimbali zilizokua zinaendelea kote duniani. Mwanaudasa mwenzetu huyu, aliweza kukiongoza chuo kwa umahiri mkubwa katika kuyafikia malengo yake bila kuathiriwa na mabadiliko yaliyokua yanaendelea ndani na nje ya chuo.

Katika kipindi cha uongozi wa Prof Luhanga, huenda ndipo UDASA ilisikika na kupata heshima ya kipekee ndani na nje ya CKD kuliko kipindi kingine chochote cha uhai wake, kutokana na wanaudasa mmoja mmoja na kama taasisi kushiriki mijadala na harakati mbalimbali kama vile kudai uhuru wa kisaisa, kupambana na rushwa nchini, kutetea uhuru wa kitaalamu, na kudai maslahi ya wanafunzi, wanataalamu, watumishi wa umma, na wafanyakazi kwa ujumla wao. UDASA ilikuwa haikai kimya kwenye changamoto yeyote iliyohusu wanafunzi, wafanyakazi, taifa, na mataifa mengine.

Sote tutakumbuka kwamba, katika kipingi cha ungozi wa Prof Luhanga UDASA iliongozwa na wanaudasa walioacha historia kubwa ya kutetea uhuru na haki za kisiasa, kiuchumi, na kisheria; walipigania maendeleo ya nchi yenye manufaa kwa wote; walipambana na ukoloni mapmboleo; walipinga rushwa; walidai na kusimamia haki na uhuru wa wanataaluma; na walidai maslahi stahiki kwa kila mtanzania. Miongoni mwao ni pamoja na Marehemu Prof Baregu; Marehemu Prof Chachage Sethy Loth Chachage; Prof Kapepwa Tambila; Prof Horub Othman; Prof Hermas Mwansoko, na mwishoni mwa uongozi wake, Dr Dalmas Nyaoro. Pia kulikua na viongozi wa DARUSO watata kama Prof Kitila Mkumbo

Katika kuelezea masikitiko ya kifo cha Prof Luhanga, mmoja wa wanaudasa amesema;

“Huyu mzee aliongoza chuo katika kipindi ambacho wahadhiri na wanafunzi wote walikuwa ni watata lakini kwa uvumilivu, usikivu na ushirikishi wa hali ya juu na bado kaacha legacy nzuri”.

Mwanaudasa mwingine ameeleza kwenye jukwaa la mijadala wa wanaudasa akisema,

“How tragic! We will remember Prof Luhanga as a man of exceptional talent, a university administrator who discharged his duties with a human touch, and a CEO who, through his innovative UDSM 2000 programme, transformed the University from the doldrums of the 1980s and early 1990s into a vibrant institution we now know it to be. We have lost a Scholar and a Professor, a Bold and Principled Leader”.

Katika kutunza heshima ya wanataalamu, uanataalama, na uhuru uhuru wa kitaaluma mwanaudasa mwingine alisema;

"Kipindi chao, academics waliheshimika sana na viongozi wa serikali na hawakuingiliwa kirahisi, wala wao hawakujipendekeza ovyo na kusahau ethics za kazi zao. This is amongst our heroes in academics and ndiyo walionifanya mimi kuipenda kazi ya academics kwa kuwa haikuwa na ku-controlled thinking ya mtu”.

UDASA tutakavyomkumbuka
UDASA itamkumbuka Prof Luhanga kutokana na uwezo wake mkubwa wa uongozi, akitumia nguvu ya hoja kujibu hoja ziliyoletwa kwake na wanaUDASA, masikilizano, na kuheshimu uhuru wa kitaaluma (academic freedom). Alipenda ukweli na haki hivyo hakuona mijadala, harakati, au madai ya wanaudasa kama tishio kwenye uongozi wa chuo au uhatarishi wa amani na utulivu wa chuo, serikali, au nchi. Hukukataa kusikiliza mawazo mbadala bali aliyapima kuona yalipopungua na wapi yana mashiko. Hata baada ya kustaafu, wana UDASA waliendelea kushirikiana naye kwa ushauri na mambo mengine ya kitaaluma na kiuongozi.

Tutamkumbuka kwa umakini na mwenye uelewa mkubwa wa mambo, ikichangiwa na tabia yake ya kusoma sana na kujiandaa kwa jambo lillilokuwa mbele yake. Hakutaka ubabaishaji, alipenda kufuata sheria, na alipenda kuona haki inatendeka. Alijiamini na kusimamia msimamo wake bila kuterereka. Hoja zilizopelekwa vikaoni bila maandalizi ya kutosha zilirudishwa ili kuwekwa sawa. Ilipobidi kuadhibu, alisimamia kile ambacho sheria za nchi, na taratibu na kanuni za uendeshaji wa taasisi vilielekeza.

Tutamkumbuka kama Mwanaudasa aliyeongoza chuo chetu kwa muda mrefu kwa uadilifu mkubwa na kuongoza bila shutuma za rushwa, wizi, au ubadhirifu wa mali ya umma.

Tutamkumbuka kwa kupenda sana kutunza muda na hakusubiri waliochelewa kufika kwenye vikao. Kwa wale aliotufundisha tunakumbuka tabia yake ya kufika darasani wiki ya kwanza ya muhula wa masomo na alipenda kuwa na kipindi siku ya Jumatatu saa moja asubuhi. Ratiba yake ngumu ya kiungozi, mikutano, safari na kusimamia mageuzi ya chuo havikumnyima kufundisha.

Tutamkumbuka kama kiongozi wa chuo aliyependa uhuru wa mawazo, uhuru wa kitaaluma, na aliyetufundisha kwa vitengo kuwa na nidhamu ya kazi, maadili, uanazuoni usiojichanganya, and respect to intellectualism and academic freedom.

Hitimisho
Kwenye jamii za kiafrika, wazee na watu maarufu kama Marehemu Profesa wanapofariki, jamii huomboleza kwa ajili yao kama naomba ya heshima kwa Maisha waliyoishi. Chinua Achebe aliyekua mwandishi maarufu, aliandika shairi kwa lugha ya Kiibo alilolilita “A wake for Okigbo”. Shairi hili aliandika kama heshima na maombolezo ya kumililia rafiki yake wa karibu sana aliyeitwa Christopher Okigbo baada ya kufariki kwenye vita vya Biafra kule Nigeria mwaka 1967. Okigbo alikua mwanashairi maarufu na Achebe alikitazama kifo chake kama kifo cha shujaa aliyekufa akitetea alichokiamini.

Achebe aliandika kusema:
For whom are we searching?
For whom are we searching?
 For Okigbo we are searching!
Nzomalizo!

Has he gone for firewood? Let him return.
Has he gone to fetch water? Let him return.
Has he gone to the marketplace? Let him return.
For Okigbo we are searching.
Nzomalizo!

[For Prof Luhanga]  
Mlimani kuna nini? Kusanyiko ni la nini!
Nijulisheni nisihamaki? yakufikirika sitaki!
Kusema hamtaki, Je niache kuhakiki?
Tafadhali nijuzeni, Namuulizia mwanaudasa

Kwa nini tumekusanyika? Natafakari!
Kwa nini tumekusanyika? Nafikiria!
Watu wanaulizia, alipo mhadhiri!
Ndiyo ni yeye, kiongozi wa wabobezi.

Profesa, Matthew mwana wa Luhanga!
Upo mtaaa upi hapa mlimani?
Mlimani kumenyamaza!
Profesa, mbona huonekani?

Wanaudasa wana kikao, Nkurumah wamekutana,
Wamealika na wageni, wana mada za mageuzi,
Wanatafuta mkaguzi, mhandisi mbobezi,
Luhanga, kwani umelala?

Profesa niambie unakuja, sema uko darasani,
Sema unafundisha Block Chain au Markov Chain,
Au niambieni una kikao, ili nikusubiri Mdigirii.
Wanaudasa wamenituma, wanataka uhariri.

Sinza road sikuoni, estate hujaenda,
Kileleni wanajenga, kukagua hujaenda,
Simba road haupo, nimetoka Kilimahewa,
Utawala nakusubiri, UDASA wana hoja.

Kijitonyama pamefungwa, kulee, CoICT ulipoanzisha,
Sheria wameketi, vitabu wanapekua,
Maktaba kumejaa, lakini hawasomi,
Nakuuliza Luhanga, kikao umeahirisha?

Ubungo house kumefungwa, Mikoresheni wamelala,
Mbugani wamenuna, Darajani kuna kilio,
UDASA kilabuni, nyimbo wamebadili,
Prof Luhanga, nakusubiri uvumbuzi.

Nahitaji msaada, kusanyiko nisaidieni.
Nachelewa kuelewa, alipo Prof Luhanga.

Je, amekwenda kuandika makala? Mwambieni arudi,
Amekwenda kuandaa kitabu? Mwambieni arudi,
Amekwenda kuhariri chapisho? Mwambieni arudi,
Wenzake twamsubiri, tuko na Mwandosya.

For whom are we calling?
For whom are we calling?
 For Luhanga we are calling.
The Hill is Silent.

Has he gone for more degrees? Let him return,
Has he gone to write a paper? Let him return,
Has he gone to write a book? Let him return,
For Luhanga we are mourning.
The Hill is Silent!

Thank you!!


Imewasilishwa na Dr Mathew Mndeme kwa niaba ya UDASA. Mathew ni Mhadhiri wa mifumo ya kompyuta na Mwakilishi wa Ndaki ya TEHAMA (CoICT) kwenye kamati kuu ya Uongozi wa UDASA kwa kipindi cha mwaka 2020 – 2022.