#
 • UNIVERSITY OF DAR ES SALAAM ACADEMIC STAFF ASSEMBLY (UDASA)

Article from UDASA member

TUCHANJE MVUA AU TUOTE JUA?
Dr Ally Mahadhy |
Published on Aug 10, 2021

Ugonjwa wa virusi vya korona (UVIKO-19), kwa mara nyengine tena unakuwa ni ugonjwa ulioleta sintofahamu kubwa kwenye jamii. Kwa hapa kwetu Tanzania sintofahamu ilianzia kwenye ujio wake, kuna watu wengi waliamini ni UVIKO-19 ni ugonjwa wa washua (matajiri), wanaopanda ndege na kusafiri nje ya mipaka ya nchi yetu. Waliamini walala hoi na wasiosafiri ugonjwa huu hauwahusu! Sintofahamu ikaibuka tena kwenye upimaji wake, mara mapapai, mbuzi na mafenesi tukaambiwa nayo yamepelekwa maabara yetu ya taifa kupimwa na yakaonekana na virus vinavyo sababisha UVIKO-19! Hii ikawa habari kubwa sana, habari ilotawala vyombo vya habari vya ndani na nje ya nchi (https://www.bbc.com/swahili/habari-52520564). UVIKO-19 bado hakuishia hapo, sasa imetuletea sintofahamu ya chanjo! Sintofahamu hii ni sintofahamu ya dunia, mkanganyiko ulioikumba jamii. Katika hili la chanjo, kuna wenye mashaka, kuna wanao shangaa, kuna waliohamanika, kuna walozubaa, kuna waliopumbazwa, kuna waliohamaki, na kuna waliofurahi.

Swali ni jee tuchanjwe au tusichanjwe?
Kabla sija jibu swali hilo (au kutoa manoni yangu) naomba nitangaze maslahi yangu binafsi kwenye mada husika. Mimi ni mtaalam na mtafiti kwenye nyanja ya bayoteknolojia (Biotechnology) mwenye shahada ya uzamivu (PhD) ya uhandisi wa kibayolojia (Bioengineering) kutoka chuo kikuu cha Lund, Sweden, nikibobea kwenye teknolojia ya vihisio vya kibiolojia (biosensor technology). Mimi ni mwajiriwa wa Chuo Kikuu cha Dar es Saalaam (CKD), Idara ya Molekyuli ya bayolojia na bayoteknolojia (Molecular biology and Biotechnology), kama muhadhiri na mtafiti; taifiti zangu zimejikita kwenye eneo la vitendanishi (diagnostic devices) vya vimelea (pathogens) vya magonjwa na viashiria vya kibayolojia (biomarkers).


Katika sintofahamu hii juu ya chanjo ya UVIKO-19, kuna hoja za msingi na rejewa ambazo zimejitokeza; ingawa kiujumla hoja zote zinagusia hoja kuu ya USALAMA (safety) wa chanjo.  Hoja za msingi na rejewa ni: muda wa chanjo (muda mfupi sana); na madhara ya chanjo (kuna walioripotiwa kudhurika). Lakini pia kuna hoja nyengine zinaibuka hapa na pale kwa lengo la kukoleza (cementing) msingi wa hoja kuu ya USALAMA WA CHANJO; mfano wapo wanaohoji kwanini iwe bure ikiwa panadoli tu tunauziwa? Kwanini tujaze fomu ya kukubali kuchanjwa (consent form) wakati chanjo nyengine hatujazi fomu? Mbona ulaya wanaandamana kupinga chanjo? Na mfano wa hoja hizo.

Ingawa kuna wataalam mbali mbali wamejitokeza kujibu hoja hizi kupitia njia tofauti, ila nikiri kwamba bado majibu au elimu hii haijawafikia walo wengi. Hii inafanya uwepo wa ulazima kwa wenye ufahamu juu ya chanjo hii kwa nafasi zao kutoa elimu kadri wawezavyo. Kwa ulazima huo huo namimi naomba nitoe maoni yangu kama ifuatavyo. Nitaaanza kwa kujibu hoja kuu mbili zilizojitokeza nazo ni: muda mfupi wa chanjo, na madhara ripotiwa! Pengine pia ntagusia na zile hoja kando kando.

Kwanini chanjo hizi zimechukuwa muda mfupi sana?
Kuna uzoefu kwamba kutengeneza chanjo au dawa mpya (vaccine or drug development) kuna hitajika miaka 10 hadi 15 hadi iweze kutumika kwa usalama na uhakika. Hii ni kutokana na hatua inazopitia, kuanzia ugunduzi na kutengeneza ndani ya maabara (discovery, development and pre-clinical trial), na wakati wa majaribio (clinical trials) ambayo hatua hii na yenyewe ina hatua (phases) hadi tano, 0 – IV (Mahan, 2014; https://www.pfizer.com/science/clinical-trials/guide-to-clinical-trials/phases). Kwa kawaida mpaka kukamilisha mchakato huo inachukua mika 10 hadi 15!  


Jee kwanini chanjo ya UVIKO-19 imekuja “fasta” hivi? Ni salama kweli?
Kwanza nianze kwa kuweka wazi kwamba hakuna sehemu yoyote inayotaka/lazimisha ili chanjo au dawa iweze kutumika lazima iwe imechukua miaka 10 hadi 15 kufanyiwa utafiti. Hii miaka 10 hadi 15, ni kutokana na uzoefu sio sheria wala kanuni! Uzoefu huu umepatikana kutokana na teknolojia na mazingira ya wakati husika. Hivyo basi kama mazingira na teknolojia yataruhusu kupatikana chanjo au dawa hata ndani ya wiki moja na mamlaka husika zikajiridhisha juu ya usalama na ufanisi wa chanjo au dawa husika, basi itaruhusiwa kutumika! Hivyo basi muda sio kigezo, kigezo ni uthibitisho wa kisayansi kwamba chanjo ni salama na ina ufanisi!


Kimazingira na kitaalamu kuna sababu (factors) nyingi zinazofanya ugonjwa upatiwe chanjo au dawa kwa haraka, hapa ntazitaja sababu chache na muhimu miongoni mwa hizo nyingi:

 1. Ukubwa wa tatizo (disease incidence, severity and prevalence)

 2. Uelewa juu ya (sayansi ya juu ya) kimelea husika cha maradhi hayo

 3. Uwepo wateknolojia inayo saidia (supporting technology) utengenezaji wa chanjo husika

 4. Maslahi katika uwekezaji (return on investment) kwenye chanjo husika


Nikianza na sababu ya kwanza ni wazi kwamba UVIKO-19 ni janga la dunia, limegusa nchi zote, tajiri sana, tajiri, maskini na hata maskini sana (Cucinotta and Vanelli, 2020). Sio kama yalivyo maradhi mengine kama malaria, ukimwi (HIV-AIDS), au kipindupindu ambayo yanajuliakana kama maradhi ya nchi maskini (Poverty Related Diseases). Hivyo ukubwa wa UVIKO-19 ambao umeathiri uchumi wa nchi tajiri na kuangamiza ule wa nchi maskini, umefanya wataalamu ulimwenguni kuingia kazini kutafuta suluhisho. Uwekezaji huu mkubwa na wapamoja wa utaalamu (intellectual investment) na kifedha, mfano badala ya kuziendea hatua za majaribio ya chanjo moja baada ya nyengine, wameziendea hatua hizo kwa pamoja (several different phases in parallel) ili kupata matokeo ya haraka, bila shaka umechangia kwa kiasi kikubwa katika upatakinaji wa chanjo hii kwa haraka, maana ugonjwa huu unagusa maslahi ya wakubwa (nchi tajiri) moja kwa moja!

Pia ieleweke kwamba kirusi cha KORONA (corona virus) si kigeni kihivyo, kama ambavyo hivi karibuni wataalamu mbali mbali wamekuwa wakieleza. Dunia ilishawahi kupigwa na kirusi cha korona kabla ya huyu wa 2019! China, Taiwan na Canada ni baadhi ya nchi zilizokumbwa na kirusi cha Korona aina ya SARS 2002- 2004 (Ruan and Zeng, 2008); na baadae akaja dada yake SARS ajulikanae kama MERS kule Saudi Arabia 2012 (Amer et al., 2018). Hivyo kuanzaia 2002 hadi 2019 yaani takribani miaka 17 tangu ajulikane SARS hadi alipokuja kaka yake, SARS-COV-2, kirusi kinachosababisha UVIKO-19 (Al-Rohaimi and Al Otaibi, 2020), wataalamu (wanasayansi) walishakuwa na uelewa wa kutosha juu ya kirusi hichi cha KORONA! Hivyo ujio wa kirusi cha UVIKO-19 haukuwakuta wanasayansi kwenye mshangao, bali walichofanya ni kujiongezea (upgrade) uelewa juu ya kirusi hicho. Hii ndo maana katika kipindi cha muda mfupi sana, tayari kulishapatikana vitendanishi vya haraka (rapid tests) na vya kijenetik (mfano “PCR”) za kila aina (Cassanit et al., 2020; Li et al., 2020; Chan, 2020; FDA, 2020)). Ingawa cha ajabu kwa hili hatukuhoji imekuaje vitendanishi (tests) hivyo vipatikane haraka?! Kutengeneza chanjo kunategemea kwa kiasi kikubwa jinsi unavyokijua kimelea kinachosababisha ugonjwa, uelewa wake wa ki-immunolojia na ki-jenetikia unarahisisha upatikanaje wa chanjo salama na fanisi! Hivyo basi uwepo wa uelewa wa KORONA aina ya SARS kumefanya kuwepo na njia za kumuelewa SARS-COV-2 kwa haraka, hivyo kumesaidia kwa kiasi kikubwa kupatikana kwa chanjo ndani ya muda mfupi, chini ya makadirio ya ki-uzoefu.

Nikielezea sababu ya tatu ya uwepo wa teknolojia saidizi; ni muhimu kuelewa kwamba ulimwengu wa teknolojia unaenda kasi sana, sio tu kwenye teknolojia ya mawasiliano na habari bali hata huku kwenye teknolojia ya uhandisi wa kibayolojia (bioengineering)! Wakati ule ambao chanjo ilikuwa inachukua miaka takribani 15 hadi kukamilika, teknolojia za ‘nanotechnology’ na seli shina (stem cells) zalikuwa bado kutimika kwenye kutengeneza chanjo na dawa; teknolojia hizi ziilikuwa ni elimu ya nadharia! Kwa sasa, ahsante kwa teknolojia hizi, hivi sasa si hadithi tena, zipo kwenye matumizi halisi ndani ya maabara zetu. Matumizi ya ‘nanoparticles’ kwenye chanjo yanasaidia kuelewa ufanisi na usalama wake katika utendaji kazi (Shin et al., 2020), hivyo kufupisha muda unatumika kwenye kujaribu njia mbali mbali za kuifanya chanjo iwe na ufanisi. Vile vile muda unafupishwa sana katika hatua ya kuelewa usalaama wa chanjo na ufanisi kwa binaadam. Awali ilikuwa chanjo ikisha jaribiwa usalama wake kwa wanyama wasio binaadamu (ambayo haihakikishi sana usalama kwa binaadamu) chanjo hiyo ilikuwa lazima ijaribiwe kwa idadi ndogo ya binaadamu ili kuelewa usalama wake, kabla ya kwenda kwa idadi kubwa na kubwa zaidi! Hivi sasa, kwa uwepo wa matumizi ya seli shina (stem cell technology) za binaadamu, inawezesha kuelewa usalama wa chanjo kwa binaadamu bila kuwepo binaadamu mwenyewe mzima (Speidel, 2021)! Seli shina hizi za binaadamu hutoa taswira halisi ya jinsi chanjo itakavyokuwa inafanya kazi na athari zake ndani ya mwili wa binaadamu. Hivyo pia teknolojia hii imesaidia sana kufipisha muda wakutengeneza chanjo ya UVIKO-19, chini ya muda wa uzoefu! Moja ya chanjo iliyohusisha seli shina za binaadamu wakati wa utengenezaji wake ni chanjo ya Johnson & Johnson’s Janssen, maarufu chanjo ya Janssen! Pia uharaka wa upatikanaji wa chanjo ya UVIKO-19 umetokana na uwepo teknolojia za uzalishaji wa chanjo (vaccine manufacturing platforms) za magonjwa ya virusi kwa muda mrefu. Teknolojia hizi zimekuwa zikitumika kuazalisha chanjo za magonjwa mbali mbali ya virusi kama ya homa za mafua ya ndege na nguruwe, ebola n.k), hivyo uwekezaji katika uzalishaji wa chanjo ya UVIKO-19 viwandani haukuwa mkubwa wala haukuhitaji muda mrefu. Hii imesaidia uzalishaji (mass production) wa haraka.

Uzalishaji wa chanjo ni uwekezaji, tena uwekezaji mkubwa sana, wa kifedha na ki-utaalamu! Tuelewe kwamba Bayoteknolojia ni Biashara pia (Entrepreneurship in Biotechnology). Hakuna anaekeza ambako hakuna faida! Tukubali tukatae, UVIKO-19 ni majanga na hasara kwa wengine, lakinia pia ni fursa kwa wengine (ikiwemo Biotech industry). Kuwekeza mabilioni ya dola kwenye kutafiti na kutengeneza chanjo ya magonjwa ya nchi maskini kama malaria, kipindupindu na HIV- AIDS ambayo wateja wake ni hao nchi masikini, ni kujitaftia hasara! Kwa hiyo usishangae chanjo ya maradhi hayo kufika hiyo miaka 15 ya uzoefu, maana pamoja na sababu nyengine za kitaalamu, lakini pia sio kipaumbele za nchi tajiri zenye teknolojia, wataalamu na rasilimani, ambao wangeweza kutengeneza chanjo za maradhi hayo kwa haraka! Lakini, hii chanjo ya UVIKO-19 soko (market share) lake ni kubwa sana, uwekezaji wake unalipa, wanunuaji ni nchi tajiri na masikini. Hivyo usilinganishe uhitaji wa chanjo hii na ile ya kipindu pindu wala HIV-AIDS katika uwekezaji! Wawekezaji na watafiti wamewekeza kadri wawezavyo katika kupata chanjo UVIKO-19 kwa muda mfupi, muda mfupi chini ya kadirio la ki-uzoefu.

Mbona kuna wanaoripotiwa kupata madhara?
Kwanza ni kuhakikishie kwamba hakuna ambacho hakina madhara, sumbuse chanjo! Lakini, chanjo hizi za UVIKO-19 kabla ya kuruhusiwa kutumika zime hakikiwa usalama wake na mamlaka husika za ki-taifa na kimataifa, likiwemo shirika la afya duniani (WHO) ambalo kazi yake kubwa ni kusimamia na kulinda afya ya binadaamu. Hivyo basi chanjo hizi hadi zimetufikia sisi kwa matumizi ni kwamba zimeshathibitiswa usalama na ufanisi wake na wataalamu kupitia mashirika husika! Ama swala la uzio (allergy) au madhara yasiyotarajiwa (side effects) ni swala la kipekee na tatizi (complex) sana, huwezi kutoa maamuzi ya kukataa chanjo kwa sababu tu kuna watu wachache walipata uzio (allergy) au madhara baada ya kuchanjwa! Jee wajua kwamba kuna zaidi ya watu 68 katika kila watu 100 hapa duniani wanaodhurika wakinywa maziwa fresh ambayo hayajaondolewa sukari aina ya lactose (Misselwitz et al., 2019); jee ulishawahi kuwaza kususia maziwa? Jee wajua kwamba si kila atakae kula karanga yu-salama? Angalau kila mtu 1 katika kila watu 100 akila karanga anadhurika (Lieberman et al., 2020). Kwani pia si wapo wanaodhuriwa na panadol (paracetamol), au dawa mseto (ALU) za malaria, au ‘azithromycin’ (na antibayotiki nyenginezo), lakini sisi wengine dawa hizo hizo zinatuponesha wala hazitudhuru! Hivyo hata kama chanjo hii ingejaribiwa kwa miaka 100 kwa zaidi ya nusu ya watu duniani, bado wangetokea ambao chanjo hii ingewadhru …kila mtu ana uzio (allergy) wa kitu flani ni vile tu hujakutana nacho bado!


Mpaka sasa dawa na chanjo zote zinatengenezwa kwa mtindo wa “saizi moja inawafaa wote” (one size fits all)! Ila kwa sababu ya uwepo wa baadhi ya watu kuitika (respond) tofauti katika matibabu au chanjo hiyo hiyo moja, kwa sasa wataalamu wameanza juhudi ya kuhusisha matibabu na vinasaba (jenetiki) vya binaadamu matibabu yawe 'personalized medicine', yaani baadae tutakuwa tunapata tiba (dawa na chanjo) kulingana na jenetiki (vinasaba) za kila mmoja wetu! Ila kwa sasa ni mwendo huu wa 'one size fits all'! Hata hivyo walioripotiwa kudhurika kwa chanjo ya UVIKO-19 ni wachache mno ya wale walochanjwa ambao wapo salama na chanjo imewasaaidia kupambana na UVIKO-19. Mfano, nchini Marekani pekee inaripotiwa kwamba mpaka kufika April 2021, zaidi ya watu milioni 8 walikuwa wameshapatiwa chanjo ya Johnson & Johnson’s Janssen (J & J/Janssen), katika hao ni watu 17 tu ndo waliripotiwa kupata tatizo la kuganda damu (Shay et al., 20201), ambayo idadi hiyo ni chini ya 0.0002 % (yaani watu 2 katika kila watu milioni moja) ya waliochanjwa kwa wakati huo. Ijulikane pia watu hao walioriporiwa kupata madhara wengi wao tayari walikuwa na maradhi mengine na ni wazee! Kwa data hizi ni dhahiri hii chanjo ni SALAMA kuliko kutokuchanjwa!

Kwanini kuchanjwa iwe salama kuliko kutokuchanjwa?
Jambo moja la msingi ni kwamba (karibia) sote tunakubali kwamba UVIKO-19 ipo! Ipo na ukiipata inatesa kimwili na kiakili (kisaikolojia), inasumbua, inafilisi, hata kuuwa! Wale walowahi kuumwa, wakawekewa mitungi ya gesi, kisha wakapona wanalo lakuhadithia, ni balaa usiombe upitishwe huko. Wale walopoteza wapendwa wao kwa UVIKO-19 wanalo lakusimulia, ni huzuni usiombe ikukute…! Ni kweli kuchwanjwa hakuku hakikishii kwa asilimia 100 kwamba hutoumwa UVIKO-19, ila kuchanjwa kuna kuhakikishia kwa asilimia kubwa kwamba hutoumwa UVIKO-19 hasa wa hizi aina zilizopo sasa. Nikama vile usivyouliza kwanini nivae kofia ngumu (helmet) wakati wapo wanaopata ajali na ‘helmet’ zao kichwani kisha wanavunjika vichwa, au nikama usivyouliza ukifunga mkanda wa gari wakati wapo wanaopata ajali wakiwa na mikanda wamefunga na wanarushwa kupitia kioo cha mbele ya gari, au unapobeba mwevuli mvua ikinyesha na bado wapo wanaorowana kwa upepea wa mvua, au kuvaa mpira wakati tendo la ndoa, na bado wapo wanaopata maradhi ya zinaa na mipira ikiwa imevaliwa….huulizi kwa sababu zote hizo kinga, hakuna kinga ya 100 %, ila pia huwezi kuacha kinga kwa kuwa tu wapo walodhurika japo walikuwa na kinga. TWENDE TUKAPATE KINGA, tujiongezee uhakika wa kutokuumwa na UVIKO-19, tusipopata kinga tunajiweka kwenye hatari kubwa ya kupata UVIKO-19! Avukae barabara akiwa amejifunika macho kwa kitambaa na yule avukae kwa tahadhari zote huku macho yake yakiwa wazi (hayajafukiwa) panauwezakano wote wakavuka salama, ila najua kamwe hutajaribu kuziba macho kwa kitambaa kisha uvuke barabara, maana una nafasi chache ya kuvuka salama! Basi usijaribu kuacha kuchanja kwa maana hutakuwa na tofauti na avukae barabara huku kafunika macho yako.


Kwanini tupewe bure?
Kuna dawa nyingi tunapewa bure, mfano dawa za kufubaza virusi vya UKIMWI, vinatolewa Au unadhani ni rahisi kuliko Panadol? Lakini pia kuna chanjo nyingi zinatolewa bure mfano chanjo ya TB, polio na nyengine nyingi. Hivyo basi chanjo ya UVIKO-19 kutolewa kwake bure haipunguzi usalama wala ufanisi wake…TWENDE TUKACHANJWE!


Kwanini tujaze fomu ya kukubali kuchanjwa, serkali inajitoa lawama?
Ridhaa (consent) ya mgonjwa ni sehemu muhimu katika maadili ya kitabibu (respect for autonomy), mara zote unapohudumiwa hospitalini au kwenye kituo cha afya umekuwa ukiulizwa ridhaa yako. Ridhaa hii inaweza kuwa ya maandishi au ya mdomo kwa mfano Daktari (mganga) kabla hajakuwekea ‘stethoscope’ kupima kifua chako, huwa anakuomba wewe mwenyewe (ridhaa yako) ufungue vishikizo vya shati lako ni baada ya kukueleza anataka kukufanyia nini, inabaki hiari yako kukubali au kukataa! Kamwe hawezi kukuvamia na kuanza kukufungua vishikizo bila ridhaa yako, anahitaji ridhaa ya mdomo! Vile vile unapofanyiwa upasuaji unajaza fomu ya ridhaa! Chanjo hii pia inakuhitaji ridhaa yako. Kuombwa ridhaa haimaanishi unataka kudhuriwa…TWENDE TUKACHANJWE!


Mbona hadi Ulaya na Marekani wanaipinga?
Hivi unajua kwamba mpaka leo kuna wanaopinga kwamba UKIMWI (HIV) hakuna ni “fix” tu? Jee wajua kwamba mpaka hii leo kuna kundi kubwa tu la watu duniani na mpaka wana chama chao wanaamini sayari yetu hii (DUNIA) ni TAMBARARE (flat) (, wewe unaamini ni duara ni mzushi tu? Jee wajuwa kwamba kuna watu wanaamini UVIKO-19 haipo ni njama za Mabeberu tu? Kila kinachoanzishwa duniani kiwe kizuri au kibaya kina wanaokiunga mkono na wanaokipinga! Hata chanjo nyengine ambazo hivi sasa tunaziona zina manufaa makubwa kama ile ya ndui (smallpox) na polio wakati wa ujio wake zilipingwa pia! Hivyo katika ulimwengu huu wa UHURU wa kidemokrasia na uhuru wa teknolojia ya habari kuwepo wanaopinga chanjo ya UVIKO-19 si jambo la ajabu wala lakutia shaka, muhimu ni HOJA zao za kupinga! Jee hoja zao ni zipi? Binafsi nimefuatilia mahojiano ya baadhi yao kwenye vyombo mbali mbali vya habari, hoja zao nyengine nizakufikirika zaidi (fiction) mfano wanaogopa kuwa mazombi (immortal) kama wakichomwa chanjo! Wengine hoja zao ni kupambania tu uhuru wao wakujiamulia wanavyotaka kuishi, hawataki kuingiliwa juu ya maisha yao (serkali zao zisiwapangie juu ya chanjo), wengine hawaamini kwamba UVIKO-19 ni hatari, wanaamini vyombo vya habari vinaongeza chumvi, hivyo hawana imani tu na chanjo! Wengine wasi wasi wao ni uslama wa chanjo, ukitoa hoja hii ambayo nimeshaitolea ufafanuzi hapo juu, hizo hoja nyengine ni ama hazihusiani na usalama au ufanisi wa chanjo yenyewe bali ni hoja juu ya utaratibu (modality) wa utowaji chanjo kwenye nchi husika au inabaki kuwa imani (na utashi) wa anaepinga chanjo; kwa mfano kama mtu anaamini atakuwa zombi wakati anajua kuna zaidi ya watu milioni 8 wameshachanjwa na hakuna hata mtu aliegeuka kuwa nusu zombi mpaka sasa, tunamsaidiaje sasa! TWENDENI TUKACHANJWE, KINGA NI BORA UVIKO-19 HAINA TIBA!
“It is better to be roughly right in due time, bearing in mind the consequences of being very wrong, than to be precisely right too late”

Makala hii imeandikwa na Dkt Ally Mahadhy ambaye ni Mhadhiri, Mtafiti, na Mhariri wa Vitendanishi (diagnostic devices) vya aina ya Vihisio vya Kibayoloji (Biosensors) katika Idara ya Molekyuli ya bayolojia na bayoteknolojia (Molecular biology and Biotechnology), Ndaki ya Sayansi Asili na Tumizi, Chuo Kikuu Dar es Salaam. Dkt Mahadhy ni mfanisi wa uhandisi wa biolojia (Bioengineering) na mweledi katika fani ya Bayoteknolojia (Biotechnology), ambaye amejielekeza kwenye tafiti za Bayoteknolojia za Matibabu na za Viwandani (Medical and Industrial Biotechnologies). Anapatikana kupitia barua pepe: allymahadhy@udsm.ac.tz au allymahadhy@yahoo.com; na kwa simu ya mkononi namba +255 (0)656 133 034.

REJEA: 

 1. Al-Rohaimi A.H, Al Otaib F (2020). Novel SARS-CoV-2 outbreak and COVID19 disease; a systemic review on the global pandemic. Gene & Diseases, 7: 491-501 https://doi.org/10.1016/j.gendis.2020.06.004.

 2. Amer, H., Alqahtani, A., Alzoman, H., Aljerian, N. and Memish, Z (2018). Unusual presentation of Middle East respiratory syndrome coronavirus leading to a large outbreak in Riyadh during 2017. American Journal of Infection Control; 46 1022–1025.

 3. Cassanit et al., (2020). Performance of VivaDiag COVID‐19 IgM/IgG Rapid Test is inadequate for diagnosis of COVID‐19 in acute patients referring to emergency room department Journal of Medical Virology, 1-4. DOI: 10.1002/jmv.25800.

 4. Chan J.F, Yip C.C, To K.K., et al (2020). Improved Molecular Diagnosis of COVID-19 by the Novel, Highly Sensitive and Specific COVID-19-RdRp/Hel Real-Time Reverse Transcription-PCR Assay Validated In Vitro and with Clinical Specimens. J Clin Microbiol. 2020;58(5):e00310-20. doi:10.1128/JCM.00310-20.

 5. Cucinotta D, Vanelli M (2020). WHO Declares COVID-19 a Pandemic. Acta Biomedica; 19 (1): 157-160. doi:10.23750/abm.v91i1.9397.PMID:32191675.

 6. FDA (2020): https://www.fda.gov/medical-devices/emergency-situations-medical.

 7. https://www.bbc.com/future/article/20210720-the-complexities-of-vaccine-hesitancy.

 8. https://www.pfizer.com/science/clinical-trials/guide-to-clinical-trials/phases/09August 2021.

 9. https://www.scientificamerican.com/podcast/episode/flat-earthers-what-they-believe-and-why/.

 10. Li et al (2020). Development and Clinical Application of A Rapid IgM-IgG Combined Antibody Test for SARS-CoV-2. Infection Diagnosis ORCID iD: 0000-0001-8854-275.

 11. Lieberman J.A, Gupta R. S, Rebecca C. Knibb R.C et al., (2020). The global burden of illness of peanut allergy: A comprehensive literature rev. Allergy; 76:1367–1384. DOI: 10.1111/all.14666.

 12. Mahan V. L (2014). Clinical Trial Phases. International Journal of Clinical Medicine; 5, 1374-1383. http://dx.doi.org/10.4236/ijcm.2014.521175.

 13. Misselwitz B, Butter M, Verbeke K, et al (2019). Update on lactose malabsorption and intolerance: pathogenesis, diagnosis and clinical management. Gut; 68: 2080–2091. doi:10.1136/gutjnl-2019-318404.

 14. Ruan L., Zeng G (2008) SARS Epidemic: SARS Outbreaks in Inner-Land of China. In: Lu Y., Essex M, Roberts B. (eds) Emerging Infections in Asia. Springer, Boston, MA. https://doi.org/10.1007/978-0-387-75722-3_5.

 15. Shay D.K, Gee J, Myers T.R (2021). Safety Monitoring of the Janssen (Johnson & Johnson) COVID-19 Vaccine – United States, March–April 2021. Weekly; 70(18);680–684. https://www.cdc.gov/mmwr/volumes/70/wr/mm7018e2.htm.

 16. Shin M.D, Shukla S, Chung Y.H, Beiss V, Chan SK , Ortega-Rivera  O.A, Wirth  D.M, Angela Chen , Sack M, Pokorski J.K and Steinmetz  N.F (2020). COVID-19 vaccine development and a potential nanomaterial path forward. Nature Nanotechnology; 15:646–655. https://doi.org/10.1038/s41565-020-0737-y.

 17. Speidel A.T (2021). Cells from human foetuses are important for developing vaccines – but they’re not an ingredient. https://theconversation.com/cells-from-human-foetuses-are-important-for-developing-vaccines-but-theyre-not-an-ingredient-157484.