#
  • UNIVERSITY OF DAR ES SALAAM ACADEMIC STAFF ASSEMBLY (UDASA)

Article from UDASA member

Ongezeko la wafanya mazoezi ndani ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam: Fursa za kitafiti
Dr Mathew Mndeme |
Published on May 24, 2021

Makala hii inatazama kwa karibu hali na mwenendo wa ufanyaji mazoezi ya kukimbia na kutembea ndani ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (CKD) na fursa za kitafiti/kisayansi zitokanayo na hali na mwenendo husika.

Mtu yeyote anayetembelea Kampasi ya Mwalimu Nyerere ya CKD kwa mara ya kwanza au ambaye hajafika ndani ya Chuo kwa miaka kadhaa, anaweza kuvutiwa au kushangazwa na mambo mengi kwa sababu mazingira ya Chuo na mambo yanayoendelea humo hayafanani na maeneo mengine ndani ya jiji la Dar es Salaam (DSM). Kwa mfano, sio rahisi kwa mtu anayejua au kusikia vurugu za jiji la DSM kuamini kwamba ndani ya jiji hili hili kuna eneo kama la CKD lenye wingi wa miti, kijani kizuri, na mapori ambayo ndani mwake kunaishi wanyama pori wasio hatarishi kwa binadamu. Kama vile haitoshi, ikitokea mtu ameingia chuoni majira ya jioni au asubuhi, kubwa analoweza kuliona kwa haraka ni idadi kubwa ya watu wanaofanya mazoezi. Iwe siku za katikati ya wiki au za mwisho wa wiki atakutana na vijana kwa wenye umri mkubwa, warefu kwa wafupi, wembamba kwa wanene, wanawake kwa wanaume: kila mmoja kivyake na kwa namna yake akifanya mazoezi. Wako wanaotembea, wanaokimbia kwa mwendo wa kujikongoja, na wanaokimbia kwa kasi kubwa. Nini fursa za kitafiti za mwenendo huu.

Ni rahisi mtu kuona wingi wa watu wanaofanya mazoezi ndani ya CKD isivyo kawaida maana, kwa utamaduni wa watanzania walio wengi, na kulingana na hali ya hewa ya joto la DSM, sio mazoea ya wengi kujituma kufanya mazoezi. Hivyo ongezeko hili linaibua swali la msingi sana la kitafiti la kutaka kujua nini sababu ya ongezeko hili na hamasa ya kufanya mazoezi ya kukimbia au kutembea. Katika kutafuta kupata majibu ya swali hili, nimekutana na nadharia mbili kuu kadhaa zinazoelezea mabadiliko haya. Moja ni madai kwamba ongezeko hili lilianza mara baada ya mlipuko wa Covid-19 kujitokeza na kupelekea   wataalamu wa afya kusisitiza umuhimu wa kufanya mazoezi kwa bidii ili kujenga kinga ya mwili. Pili, ni maelezo kwamba watu wengi wanafanya mazoezi sio kwa kusukumwa na umuhimu wa kuimarisha afya zao bali kwa msukumo wa mitandao ya kijamii kwa lengo la kujionesha mitandaoni.

Ni jukumu la tafiti kutafuta kujua nini chanzo cha ongezeko la wanaofanya mazoezi ndani ya CKD na iwapo ongezeko hilo linaashiria ongezeko la uelewa wa umuhimu wa mazoezi katika kuimarisha afya au kama kuna sabau zingine. Ni utafiti pekee unaoweza kuonesha mwelekeo wa ongezeko hilo ukoje na  kama kuna mambo yanayoathiri mwelekeo huo. Pia. Utafiti unaweza kuonesha ni kundi gani miongoni mwa wanaofanya mazoezi ndani ya CKD linaonekana kuwa na mwitikio zaidi kwa vigezo kama vya umri, jinsia, na hali za afya. Maswali haya ya kitafiti yatakata kiu ya kupata majibu ya kisayansi na uelewa mpana wa sababu zinazoepelekea mwitikio mkubwa wa watu kufanya mazoezi.

Swali lingine linalohitaji majibu ya kitafiti ni la kimazingira na miundombinu. Uwepo wa watu wengi wanaofanya mazeozi ndani ya CKD ni rahisi kumfanya mtu afikiri kwamba wafanyakazi na wanafunzi wanapenda sana mazoezi. Hata hivyo ukifuatilia kwa karibu utagundua wanaofanya mazoezi ndani ya CDK sio watumishi, wakazi, na wanafunzi wa CDK peke yao. Wako wanaotoka huko watokako kwa magari kisha wanayaegesha nje au ndani ya Chuo na kufanya mazoezi. Utafiti utatupa fursa ya kuelewa iwapo kinachowavutia na kuwahamasisha wanajumuiya kinafanana na ile ya wakazi wa nje ya CKD. Pia, utafiti utajibu swali la iwapo mazingira na miundombinu ya CKD, kwa namna moja au nyingine, yanaongeza hamasa ya kufanya mazoezi na kuchangia kuongezeka kwa wanaofanya mazoezi.

Pamoja na tafiti za kisayansi kuonesha umuhimu wa kufanya mazoezi kwa bidii, mazingira na miundombinu ya kufanya mazoezi nayo yana mchango katika manufaa ya kufanya mazoezi. Kwa mfano, inajulikana vema kuwa magari na vyombo vingine vya moto vinavyotumia mafuta vinatoa gesi chafu za kaboni zenye madhara kwa afya zetu. Gesi hizi zinachafua mazingira na tunapotemba pembeni mwa barabara zinatuathiri kwa karibu zaidi. Hata hivyo mtu anapokua anafanya mazoezi, anavuta hewa kwa nguvu na kwa kasi zaidi ili kuwezesha mifumo ya mwili wake kufanya kazi vema na kupata nguvu ya kutosha. Kwa minajili hiyo hiyo, mtu anayefanya mazoezi barabarani anavuta hewa yenye mchanganyiko na gesi zenye sumu kwa wingi zaidi. Iwapo wewe  hufanya mazoezi ya kukimbia , unaweza kuelezea vema tofauti kubwa ya upumuaji unapokimbia barabarani kunapokua na magari na unapokimbia kwenye njia zisizo na magari. Hivyo pamoja na manufaa ya kufanya mazoezi, yanapofanyika katika mazingira yenye gesi za kaboni, vumbi, na uchafu mwingine kwenye hewa mtu anayofuta, kuna uwezekano mkubwa wa kupata madhara mengine kiafya. Hivyo Kwa kua kua idadi kubwa ya magari yanayopita ndani ya CDK kuelekea na kutoka maeneo kama Ubungo, Msewe, Changanyikeni, Goba, Makongo, Ubungo na kwingineko, kuna uwezekano mkubwa kwamba   wanaofanya mazoezi katika barabara ya CDK kudhurika na gesi chafu na vumbi vitokanavyo na magari. Ni jukumu la wanasayansi wa CKD kubuni utafiti unaonesha ni kwa kiasi gani mtu anayefanya mazoezi katika mazingira haya yuko katika hatari ya kupata madhara pamoja na kwamba anatafuta faida ya kiafya.

Swali la mwisho la kitafiti linaloweza kujibiwa na fursa ya kinachoendelea ndani ya CKD, ni la usalama wa wanaofanya mazoezi dhidi ya magari na tabia za uendeshaji magari ndani ya CKD. Wakati mwingine unaona wazi jinsi wafanya mazoezi wanavyopishana na magari kwa shida au waendesha magari wasivyowajali wale wanaofanya mazoezi na kuwapa wasiwasi mkubwa wa usalama wao.  

Maswali yote ya kitafiti niliyoainisha hapo juu na mengine yanayoweza kujitokeza, yatasaidia sana mikakati ya nchi katika uimarishaji wa afya ya jamii. Matokeo ya tafiti hizi yatatoa majibu ya kisayansi kuhusu nini vichocheo vya hamasa ya kufanya mazoezi ya kukimbia na kutembea kwa makundi mbalimbali na ni kwa jinsi gani vichocheo au hamasa hizo zinaweza kutumika kushawishi watu na makundi mbalimbali na mazingira tofautitofauti kufanya mazoezi zaidi. Pili, tafiti zitatusaidia kuelewa kisayansi kwa nini kuna ongezeko la wafanya mazoezi katika mazingira ya CKD na iwapo ongezeko hilo ni endelevu au ni la msimu. Majibu haya yatasaidia kutoa ushauri kwa CDK, taasisi nyingine zenye mazingira kama ya CKD na kwa mamlaka za nchi namna ya kutenga na kuandaa mazingira rafiki ya kuhamasisha ufanyaji wa mazoezi ya mwili. Hii ni pamoja na kushauri aina ya miundombinu wezeshi na salama kwa afya na usalamawa wanaofanya mazoezi. Tatu, tafiti zitaonesha kiwango cha gesi na vumbi chenye madhara kitokanacho na kufanya mazoezi sambamba na barabara za magari na muda ambao unaweza kuwa salama zaidi kwa wakimbiaji. Hii inaweza kuwa ni pamoja na kushauri njia mbadala za kufanya mazoezi yenye manufaa bila kudhurika.

Nne, manufaa mengine ya tafiti zinazohusu wafanya mazoezi ya kukimbia na kutembea ndani ya CKD yanaweza kuwa ya ngazi ya kitaasisi. CKD kinaweza kupanua wigo wake wa kitafiti na uwekezaji kwenye eneo la elimu ya mazeozi (physical education) kwa kubuni mazingira rafiki ya kufanya mazoezi na kuingizia taasisi mapato ya huduma zinazoweza kutolewa . Hii yaweza kuwa ni pamoja na kutumia vizuri eneo kubwa la chuo kutengeneza maeneo maalumu ya kufanyia mazoezi mbalimbali kulingana na uhitaji wa watu; kulifufua na kuliboresha bwawa la kuogelea linalohitajika  sana; kuboresha na kupanua barabara zake kwa kuziongezea njia maalumu za waenda kwa miguu; kuongeza wingi wa taa za barabarani na maeneo mengine yote ndani ya Chuo ili kuyawezesha kutumika vema mchana na usiku, kulingana na ratiba za watafuta huduma; kujenga ukumbiwa kisasa wa mazoezi ya viungo (gym) na kuongeza ubora na  ukisasa na kupanua wigo wa huduma nyingine ndani ya Chuo kama za afya katika kituo cha afya cha CKD, chakula, vinywaji na duka la vifaa vya mazoezi na michozo.

Tano, majibu ya maswali haya ya kitafiti yanaweza kuchangia kutoa mawazo ya kisayansi ya namna ya kuboresha usalama barabarani na ushauri unaoweza kutumiwa na Wizara ya Afya na wadau wengine katika uboreshaji wa mikakati ya kuhamasisha ufanyaji wa mazoezi na kupambana na magonjwa nyemelezi yanayoweza kuzuilika kwa kujenga mazeoa  ya kufanya mazoezi.

Makala hii imeandikwa na Mathew Mndeme ambaye ni Mhadhiri, Mtafiti, na Mchambuzi wa Mifumo ya TEHAMA katika Ndaki ya TEHAMA ya CKD. Pamoja na maeneo mengine, amejielekeza katika tafiti zihusinazo matumizi ya mifumo ya kidigitali katika kuboresha Afya ya Jamii, kukabiliana na magonjwa ya kuambukiza, na kuboresha usalama barabarani. Anapatikana kupitia mathewmndeme@udsm.ac.tz / mathewmndeme@gmail.com na kwa simu ya mkononi 0788835883.