#
  • UNIVERSITY OF DAR ES SALAAM ACADEMIC STAFF ASSEMBLY (UDASA)

Article from UDASA member

Jinsi Elimu Inavyochochea Umasikini Nchini Tanzania
Dr Armstrong C. Matogwa |
Published on May 24, 2021

Utangulizi
Katika malezi yetu tumefundishwa kwamba elimu ni kitu cha thamani sana. Ili kudhihirisha thamani hiyo wahenga wetu walifanikiwa kutunga misemo mbalimbali ili kuonesha dhahiri umuhimu wa elimu na hasa elimu rasmi. Baadhi ya misemo hiyo ni “elimu ni ufunguo wa Maisha”, “kama unaona elimu ni ghali jaribu ujinga”, “mizizi ya elimu ni michungu lakini matunda yake ni matamu”. Pamoja na misemo hii walimu na wasanii pia wamejaribu kutunga nyimbo mbalimbali ili kutukumbusha umuhimu wa elimu. Kwa mfano, katika madarasa ya awali tuliimba wimbo usemao “asiyejua kusoma ni mjinga kabisa, barua ikija aitembeza kutwa”. Pia mwanamuziki Samba Mapangala aliwahi kuimba kwamba “somesha mtoto shule, apate elimu, atafaidika kwa maisha yake”. Misemo hii na na nyimbo hizi vinajaribu kudokeza thamani kubwa ya elimu katika maisha yetu, na kwamba bila elimu ni vigumu kupata maendeleo.

Hata hivyo, pamoja na thamani hiyo kubwa, uzuri na umuhimu wa elimu katika malezi yetu, hatuambiwi ubaya wa elimu hiyo. Hapa sina maana ya kusema kuwa kila kitu kina uzuri na ubaya wake, la hasha! Lengo langu ni kueleza kuwa katika mazingira tuliyonayo elimu hii rasmi, kwa sehemu kubwa inachochea umasikini na kudidimia kwa taifa na si vinginevyo. Jambo hili linajidhihirisha wazi kwa kuchambua maudhui ya elimu yetu kwa kulinganisha na mazingira yetu pamoja na matarajio/matamanio yetu kama taifa. Katika Makala haya nitaeleza kwa kifupi jinsi ambavyo elimu tunayoipata shuleni/vyuoni haiendani na muktadha wetu na malengo yetu, na hivyo kurudisha nyuma jitihada za taifa katika kujikwamua na umasikini na unyonge.

Tafakuri juu ya umasikini
Umasikini ni moja kati ya matatizo yanayofanyiwa sana utafiti duniani kote. Kutokana na hali hiyo kumekuwepo na dhana mbalimbali kuelezea hali na kiasi cha umasikini. Kwa mfano, kunawanaoelezea umasikini kama ni ukosefu wa kipato, wengine huona umasikini kama ukosefu wa chakula, wengine huutazama umasikini kwa jicho la ukosefu wa ukuaji wa uchumi. Katika makala hii dhana ya umasikini imepanuliwa zaidi ili kueleza mambo katika uhalisia wake. Hapa umasikini wa taifa umeelezwa kama hali ya kukosa maendeleo na kuwa duni katika mambo ya msingi. Haya yote yanajidhihirisha na uduni wa zana za uzalishaji mali kama vile viwanda, ardhi, maliasili na nguvu kazi. Maendeleo katika zana za uzalishaji mali ndiyo maendeleo halisi; na kinyume chake, kutokuendelea kwa zana za uzalishaji mali, ndiyo chanzo cha umasikini. Hivyo basi umasikini uwe wa kipato, wa chakula ama kutokukua kwa uchumi ni sehemu tu ya vielelezo vya umasikini na si canzo cha umasikini wenyewe.

Aina hii ya umasikini haikuwepo Afrika, imeletwa na wageni (Waarabu na Wazungu) hasa kuanzia karne ya 16 ambapo waliendesha biashara ya utumwa katika bara la Africa. Kabla ya ujio wa Wazungu, Afrika ilikuwa imeendelea katika zana za uzalishaji mali, kulikuwa hakuna utegemezi kati ya jamii na jamii. Waafrika walipiga hatua za kiuzalishaji, kutoka kutumia zana za mawe mpaka zana za chuma ambazo zilisababisha kuongezeka kwa uzalishaji na kupanuka kwa himaya zao. Kwa kuwa kila mtu alikuwa na ardhi na aliweza kupata zana za uzalishaji mali hiyo ilitosha kuwafanya watu wasiwe masikini. Baada ya kuingia kwa ukoloni, maendeleo ya zana za uzalishaji mali yalidumazwa. Wakoloni walipiga marufuku uzalishaji wa zana za chuma na adhabu kali ilitolewa kwa waliokamatwa. Hivyo basi Waafrika walilazimishwa kununua zana za uzalishaji mali kutoka Ulaya. Hii iliua kabisa fikra na ujuzi wa kutengeneza dhana mbalimbali za kuzalishia mali. Hivyo ukoloni uliweka msingi wa umasikini na utegemezi wa fikra na maendeleo. Tangu wakati huo Waafrika walilazimishwa kuamini kuwa maendeleo yanatoka Ulaya, Wazungu ndio pekee wanaweza kutengeneza vitu bora, Wazungu ndio pekee wenye teknolojia, hatuwezi kuishi vizuri bila kuwategemea Wazungu, Wazungu ni bora kuliko sisi, Wazungu wana upendo sana, Wazungu wamekuja ili kutusaidia, maendeleo ya kweli yako Ulaya na kila kitu kizuri kiko ulaya, Waafrika hatuwezi kuendelea mpaka tuige utamaduni, elimu na mambo ya Ulaya.

Japokuwa wakati wa ujamaa Watanzania walipambana kuupinga ukoloni, fikra hizi zimeendelea kudumu hata sasa. Leo hii fikra hizi za utegemezi na uzunguishaji (dependency and eurocentrism) zimo katika mitaala, silabasi na vitabu vya kiada wanavyotumia walimu na wanafunzi wetu. Ni kama vile taifa limekubali kudidimizwa kwa zana zetu za uzalishaji mali. Fikra hizi (ambazo zilipandikizwa wakati wa ukoloni na zinadumu hadi leo) ndizo zilididimiza maendeleo ya zana hizo na hata kusababisha umasikini na utegemezi. Kwa maneno mengine japokuwa taifa limekuwa likisambaza elimu kwa Watanzania, lakini elimu hiyo ndiyo imekuwa nyenzo kubwa ya kuchochea umasikini na utegemezi. Hili ni tatizo. Si tatizo la elimu tu bali ni tatizo la maarifa. Tatizo hili haliwalengi wanafunzi wanaofeli tu, au wasiosoma, bali ni tatizo la Watanzania wote; na kibaya zaidi kwa siku za hivi karibuni, jinsi mtu anavyosoma zaidi ndivyo anavyojiongezea tatizo. Hali hii imesababisha mpaka leo taifa letu halina maendeleo kwa sababu “elimu yetu haina maarifa” yanayotuwezesha kuendeleza zana zetu za uzalishaji mali, matokeo yake tunaishi tukitegemea zana bora kutoka Ulaya na sasa China. Watanzania tumeshindwa kutengeneza hata majembe ya mkono pamoja na kwamba tuna madini ya chuma kule Liganga na Mchuchuma. Mengi ya majembe bado yanatoka China na tangu kabla ya ukoloni mpaka leo wakulima wetu wanatumia jembe la mkono. Sekta yetu ya viwanda imeendelea kuwa tegemezi, inategemea teknolojia na wataalamu kutoka nchi za nje. Hii ni kuendeleza elimu waliyotupa wakoloni ambayo ilitufanya kuwa masikini, kuwa tegemezi, na kuwaona wao ni bora sana kuliko sisi.

Maarifa ya utegemezi na umasikini katika elimu yetu
Katika masomo mengi yanayofundishwa hapa nchini Tanzania kuanzia ngazi ya shule ya msingi mpaka chuo kikuu, hali ya utegemezi imetawala sana. Kwa mfano, katika masomo ya Urai, Historia, Baolojia, Fizikia, nk (Civics, History, Biology, Physics, etc) sehemu kubwa ya maarifa hayo hayamwezeshi mwanafunzi kutafakari juu ya mazingira yanayomzunguka bali hulazimika kukariri kile kilichoandikwa vitabuni ambacho hakiakisi mazingira yake. Maarifa haya si tu hayamsaidii mwanafunzi kutafakari mazingira yake bali hufanya kazi ya kumpumbaza na kumfanya kiumbe asiyefaa, asiye na maarifa na asiyejua kitu. Hatimaye mwanafunzi huyu anajengewa hali ya kutegemea wenye maarifa kutoka nje ya Afrika maana huko  ndiko kwenye maarifa na kweli.

Katika somo la uraia (Civics) kwa mfano kuna mada kama za Human Rights (form I), Democracy, (form II), Gender (form II), Economic and Social Development (form III), na Culture and Globalization (form IV); hizi zimejaa maarifa yanayojenga utegemezi kwa wanafunzi wetu – maarifa yanayowatenganisha wanafunzi na mazingira yao.  Mada hizi zote zimejengwa katika misingi ya uliberali mamboleo, falsafa ambayo lengo lake ni “kuharibu” maisha ya Watanzania na Waafrika kwa ujumla. Kwa mfano mada za Haki za Binadamu (Human Rights) na Demokrasia (Democracy) zimeandikwa bila kuzingatia historia ya Tanzania na bara la Afrika kwa ujumla, na pia zimeandikwa bila kuzingatia uonevu wa kitabaka wa kitaifa na kimataifa, na kwa jinsi hii mada hizi zinasambaza maarifa yasiyoendana na mazingira yetu. Japokuwa kwa juu juu zinaonekana kama zinaeneza maarifa mazuri, yenye upendo, yanayofaa sana, lakini ukiangalia kwa undani utaona jinsi zinavyopotosha historia yetu na jinsi zisivyoendana na mazingira yetu. Mada hizi, katika elimu ya sekondari hata chuo kikuu hazielezi mambo muhimu kama maslahi ya kisiasa na kiuchumi yaliyomo katika maarifa hayo; mfano, ni nani aliyeleta haki za binadamu na demokrasia? Je, Haki za binadamu ziko za aina moja tu? Je, ni lazima watu wote dunia nzima tuzifuate hizo haki za binadamu kama vile zimetoka kwa Mungu? Je, ni kipi kinasababisha haki hizo kuwa takatifu? Kwa nini haki za binadamu na demokrasia zinaruhusu matabaka (social classes) katika jamii? Je, matabaka ni kitu kizuri? Je, demokrasia iko ya aina moja tu dunia nzima na lazima wote tuifuate hiyo?

Kwa kuzingatia maswali haya utaona kuwa maarifa yanayosambazwa na mada hizi na somo zima la uraia (Civics) yanalenga kuhalalisha kuwa uliberali mamboleo ndio mfumo wa maisha unaofaa duniani na kwamba nchi zote duniani ikiwemo Tanzania ni lazima kuufuata. Mfumo huu wa uliberali ndio umezalisha maarifa ya uliberali mamboleo ambayo ndiyo yanayotawala katika shule na vyuo vyetu. Maarifa haya yamezalishwa katika nchi za kibeberu (central capitalism) na kusambazwa duniani kote kwa lengo la kulinda maslahi ya kibeberu. Kwa hiyo, maarifa ya Haki za binadamu, Demokrasia, Jinsia, Maendeleo na Utandawazi kama ambavyo yameandikwa katika vitabu vya shule za sekondari na vyuo vikuu ni maarifa ya kibeberu, yaliyozalishwa kwa kuzingatia mazingira ya nchi hizo (central capitalist nations) na maslahi yao. Maarifa hayo hayajazalishwa ili kuwasaidia Waafrika au Watanzania, kwa sababu ni maarifa ambayo hayatokani na mazingira ya Africa.  Haya si maarifa yanayotetea na kulinda maslahi, heshima, utu na utamaduni wa Waafrika/Watanzania bali ni maarifa ya kuwatukuza Wazungu, kuwakweza na kuwahalalisha mabeberu kuwa wao ndio watawala wa maarifa na watawala wa siasa na uchumi duniani.

Katika masomo ya sayansi kwa mfano ni jambo la kushangaza kuona kuwa kila maarifa ya sayansi yameanzia Ulaya.  “Physics comes from the Greek word Physikos which means natural…..“The word ‘Biology’ comes from two Greek words; bios and logos…. Maneno haya ambayo huanza katika utangulizi wa somo la physics na biology humuandaa mwanafunzi wa Tanzania kuelewa kwamba sayansi ni maarifa yanayotoka nje ya Afrika. Hata nadharia mbalimbali zinazofundishwa katika shule za sekondari kwa mfano ni nadharia za kigeni/Wazungu. Masomo yanafundisha Archimedes principles, Newtons law of motion, n.k. Kwa ujumla mambo haya yote yanamwambia mwanafunzi wa Tanzania kwamba sayansi imetoka Ulaya na Waafrika hawajawahi kufanya jambo lolote la kisayansi; na kwamba Afrika tangu enzi na enzi hakuna sayansi wala wanasayansi. Maarifa haya si tu yanamfanya mwanafunzi wa Tanzania kuwa tegemezi na mnyonge lakini pia yanapotosha ukweli. Historia ya Afrika inaonesha ni jinsi gani Waafrika walivyokuwa wanasayansi na kutengeneza nyenzo na vifaa vingi vya kisayansi. Tangu miaka 300 K.K waafrika wamekuwa wakijihusisha na kilimo cha umwagiliaji, unajimu, elimu ya hesabu, elimu ya falsafa, ujenzi (mfano piramidi za Misri), utengenezaji wa ngalawa na meli, kutibu wagonjwa wa kila aina, kufanya upasuaji nk. Lakini cha ajabu mambo haya yote ya kisayansi hayafundishwi popote katika masomo yetu. Japokuwa elimu ya Unajimu imeanzia Afrika lakini ni jambo la kushangaza kuona katika mada ya unajimu kwenye vitabu vyetu vya physics havisemi chochote kuhusu Afrika na Waafrika. Zaidi, vitabu vinaandika kuwa Wazungu walitumia elimu hiyo kusafiria basi.  

Kwa namna hii elimu tunayoipata inatusababisha kuwa masikini kwa sababu haitufundishi kutafakari mazingira yetu na historia yetu bali kukubali na kutukuza maarifa ya wengine. Maarifa haya hayahoji unyonyaji na ukandamizaji unaofanywa na mabeberu kwa takribani karne 5 sasa. Maarifa haya hayatusaidii kupiga hatua za kimaendeleo kwani yanatufundisha kuishi kama mabeberu wanavyotaka, na sio kupambana nao. Mfano, kuwaruhusu mabeberu kuiba rasilimali zetu inaonekana ni sawa lakini kuwakamata na kuwakataza wasiibe inaonekana ni uvunjaji wa haki za binadamu. Kwa maarifa haya inaonekana ni kitendo cha kidikteta kusimamia rasilimali za taifa zisiibwe, kusimamia miradi ya maendeleo ya taifa lakini ni demokrasia kuacha rasilimali hizo zipotee na nchi kuishi kwa kuwategemea Wazungu na kuomba misaada kutoka kwao. Maarifa haya yanatufundisha kuwa ni burasa kuishi kwa kuomba misaada lakini ni uvunjifu wa demokrasia na haki za binadamu kwa nchi kutafuta kujitegemea. Maarifa haya ni kichocheo cha umasikini wetu na umasikini kwa taifa letu.

Hitimisho: Je, Tatizo ni Elimu au Maarifa?
Katika siku za hivi karibuni kumekuwa na mjadala mkubwa juu ya ubora wa elimu nchini Tanzania. Watanzania wengi hawaridhishwi na elimu yetu na hivyo wamejikuta wakiikosoa kila kukicha. Lakini wengi wetu wanaposema elimu mbovu humaanisha wanafunzi hawafundishwi vizuri, vitabu havitoshi, wanafunzi wanakaa chini, wanafunzi wengi hawafaulu kwenda sekondari au vyuo vikuu, mtaala mbovu, sera ya elimu haifai n.k. Inawezekana haya yakawa ni sehemu ya kile kinachoitwa tatizo la elimu Tanzania. Katika Makala haya nimejaribu kuonesha sehemu kubwa ya tatizo letu ni maarifa, na sio elimu. Maarifa yanayozalishwa na kusambazwa na mfumo wetu wa elimu yamejaa utegemezi, unyonge na utukufu kwa Wazungu. Maudhui ya masomo yetu hayawapi Watanzania heshima na utu; bali unyonge na kushindwa. Kwa sababu hiyo, Watanzania tumeshindwa kutafakari mazingira yetu (social context) sawasawa na kwa miaka mingi sasa, tunaishi katika hali ya kutegemea misaada kutoka nje ya nchi.

Dr Armstrong C. Matogwa ni Mhadhiri katika Idara ya Sosholojia, Chou Kikuu cha Dar es Salaam